IPTL Serikali Ikiri Kushindwa

Hivi karibuni, serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ilitoa mpya ya mwaka katika harakati zake za kuendelea kubariki na kuhalalisha haramu ya wazi. EWURA iliwataka watanzania kutoa maoni yao juu ya ima kampuni kidhabi la independent Power Tanzania Ltd (IPTL) lipewe leseni ya kuendesha hujuma yake au la. Bila kujali wala kukumbuka kuwa watanzania wanajua kuwa IPTL ni serikali ndani ya serikali tena iliyoendelea kujitanua nchini bila ya hata kuchaguliwa. Imekuwa madarakani kwa vipindi vitatu bila kuchaguliwa tangu ilivyoingizwa nchini kimezengwe mwaka 1995 chini ya awamu ya tatu ikiwagusa moja kwa moja marais wastaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete.

Meneja wa Mawasiliano wa EWURA, Titus Kaguo alikaririwa akisema “Ewura tunapokea maoni ya wananchi kwa maandishi, kwa hiyo litakuwa jambo la kizalendo kwa wananchi kujitokeza kutoa maoni yao ama kupinga IPTL au kuunga mkono ili itusaidie nasi kufanya maamuzi.” Kwanza, huyu Kaguo sijui kama niiptl mtanzania; na anajua maada ya uzalendo. Kwanini EWURA wawatake wananchi kutoa maoni sasa na si wakati wakiiingiza balaa hili nchini? Nini kimebadilika hadi wananchi kuwa na maana wakati walishaibiwa miaka nenda rudi ukiachia mbali kulalamika bila kusikilizwa kwa muda mrefu? Ni bahati mbaya kuwa EWURA imetoa maelezo kidogo kiasi cha kuacha maswali mengi bila majibu. Mfano, wanatumia sheria gani kutaka maoni ya wananchi; na wananchi watakuwa na hakikisho lipi kuwa maoni yao hayatachakachuliwa au kutumika kuhalalisha jinai hii ya muda mrefu?

Kwa wanaojua ukubwa wa hujuma iliyofanywa na IPTL na makuwadi wake wa nchini, wanashangaa upendo, uwazi, ushirika, ushirikishwaji, ushikaji hata ushidau na udau vimeanza lini na kwa nini?     Wapo wanaodhani kuwa hii ni janja ya walaji wenye madaraka walioshirikiana na kampuni hii kwa muda wote ambao imekuwa ikiliibia taifa kuwaingiza mkenge mwingine watanzania kwa kuwashirikisha kwenye jinai hii ambayo imewatesa watanzania kwa muda mrefu. Rejea kuendelea kuhujumiwa na kudhoofishwa kwa Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) ambalo wezi walioko nyuma ya jinai hii wamekuwa wakiikamua fedha kiasi cha kuilazimisha kuwatwisha mzigo wateja wake bila huruma.

Je watanzania watakubali ghilba hii ya kutaka kuwafanya sehemu ya jinai hii ya kikatili? Je hata wakitoa maoni yao yataheshimika? Nani anamdanganya nani na nani anataka kumtumia nani katika dhambi hii ya kuhujumu taifa? Je EWURA wana nguvu gani kisheria kuanzisha mchakato huu wa mashaka? Je ni kwanini serikali inajitoa kiasi cha kuachia taasisi ndogo kama EWURA wakati ina mamlaka ya kuingilia kama ilivyofanya kwenye sekta ya madini? Je hii ni namna ya serikali kuficha sura au dalili za kukiri kuwa IPTL haigusiki kiasi cha kuwa kama serikali ndani ya serikali? Kwanini serikali isiunde tume maalum ya wataalamu ya kuchunguza jinai hii ya muda mrefu? Mbona makampuni mengine ya kigeni hayapitii mchakato kama huu wenye kuhitaja maoni ya watanzania?

Kwa vile rais John Magufuli ameonyesha kuwa na uzalendo na uchungu na raslimali za taifa, tunashauri aingilie kati kuondoa upuuzi huu wa kutaka maoni ya wananchi wakati hayana nguvu kisheria. Magufuli amekuwa mwepesi kushughulikia kadhia mbali mbali kama vile ujenzi holela, wizi bandarini, vyeti feki na ajira hewa, madini na mengine; ingawa anaonyesha kusuasua au kukaa kimya kwenye sakata la IPTL ambalo lina maslahi makubwa kwa taifa hasa ikizingatiwa hujuma ambayo IPTL imekuwa ikifanya nchini kwa muda mrefu. Je Magufuli anachukulia kashfa hii kama kaburi kwa vile walioiasisi na kuitumia ni baadhi ya watangulizi wake ambao aliwaahidi ulinzi dhidi ya kashfa mbali mbali zinazowakabili? Hadi sasa hakuna anayeweza kueleza ni kwanini Magufuli anasitasita kukaa kimya kuhusiana na kashfa hii yenye madhara makubwa kwa maisha ya watanzania.

Wengi wanahoji: kwanini EWURA wanataka maoni ya watanzania wakati hawajui kilichoko kwenye mikataba yao na IPTL? Je EWURA wako tayari kuweka wazi mikataba hiyo kwa kuipeleka bungeni ili wawakilishi wa wananchi waione na kuridhia au kupinga kilichopo kabla ya kutaka maoni ya jumla yanayolenga kuhaendelea kuhalalisha uwepo wa IPTL nchini ikifanya hujuma ile ile ambayo ni hatari kwa usalama wa taifa? Kwanini EWURA wasiitake serikali kupeleka mswaada wa sheria bungeni kuangalia namna ya kuondokana na donda ndugu na jinamizi hili liitwalo IPTL?

Tumalizie kwa kuwataka EWURA waache kutuhadaa kwa kutaka kulinda maslahi ya wezi wachache wenye mamalaka. Huu umchakato wa kutaka maoni unapaswa kulaaniwa na kusimamishwa ili kuangalia namna bora ya kushughulikia jinai ya IPTL kwa kuwakamata wote waliohusika na hujuma hii, kuwafilisi na kuwafikisha mahakamani huku mitambo ya IPTL ima ikikamatwa au kutoipa kampuni hii leseni nyingine ya kuendelea kuwaibia wananchi wasio na hatia. Rais Magufuli, tafadhali, simamisha ghilba hii na utumbue IPTL na wote walioko nyuma yake. Haiwezekani Tanzania iendelee kugeuzwa kichwa na mwendawazimu na matapeli wa ndani na nje kwa kisingizio cha uwekezaji ambao kimsingi, ni uchukuaji na ujambazi wa mchana kweupe.

Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho.

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s