Kijiwe Kupeleka Maazimio Yake Ewuuura

Baada ya kuzinyaka kuwa kuna zengwe la kutaka kuwashirikisha wachovu kwenye wizi mwingine chini ya ujambazi wa IpTL, kijiwe kimekaa kama kamati ya uokozi ili kutoa mwelekeo wa namna ya kuzuia na kukomesha wizi huu donda ndugu.Msomi Mkatatamaa analiamsha dude kwa kufichua kile alichodurusu kwenye gazeti fulani ambalo leo hatutaji jina. Anasema “wasomi wanakijiwe, nimeinyaka kuwa mamlaka ya ulaji wa angani, ardhini na majini ina mpango mchafu wa kutaka kutuhusisha kwenye jinai yake ya kuendelea kubariki wizi wa IpTL.” Anatoa gazeti na kuliweka mezani na kuendelea “hebu angalieni wanavyodai tutoe maoni yetu kabla hawajaruhusu wizi huu kuendelea kama njia ya collective consent au uhusika wa umma katika kuhalalisha haramu hii donda ndugu. Sijui hawa wezi wanataka kutumia sheria gani wakati kila kitu kiko wazi kuwa IpTL ni jipu ambalo rais Kanywaji anapaswa kulitumbua haraka. Hata sijui kwanini amekuwa mwepesi wa kutumbua majipu mengine kuanzia Bandarini, Uwanja wa ndege, Madini na kwingineko lakini anaigwaya IpTL utadhani nayo ni Bashite!”

“Kweli hapa kazi tu na ipo kazi kweli kweli! Yaani baada ya kulala kitanda kimoja miaka yote hii wakifanya ufuska wao wametuchoka kiasi hiki hadi kutaka tubariki haramu hii! Wallahi mie simo na kama nimo basi nitatibua dili zima. Nadhani hapa dokta Kanywaji anatanivumilia kusema kuwa hili ni jipu lake analopaswa kulitumbua. Kama akishindwa ajue amejitibulia vibaya sana. Maana alisema hataogopa wala kumuonea mtu. Je inakuwaje anaendelea kufumbia macho ujambazi huu wa wazi?” anachomekea Kapende huku akitafuna meno na kusonya kwa hasira.

Kabla ya kuendelea kudema Mpemba anampoka mic “yakhe nami nkubaliana nawe. Yanini walete hii kitu leo wakati wamekuwa wakitutafuna pamoja bila kujali? Je haya mapenzi yantoka wapi au wantakaendelea tuchafua na kutuibia kama kwamba sie ni hamnazo kama wao waliojilegeza na kuachia kula kitu utadhani vyangu au hamnaazo? Kula mmeisha kula eti mnataka tutoe mawazo wakati mnaosha vyombo; ile iweje?”

Mipawa hajivungi. Anakwanyua mic “kwanini sasa na si nyuma na mbona huko nyuma hawakuwa hivi? Kwanini wametangaza upuuzi huu kwenye gazeti binafsi kana kwamba government gazette haipo? Hapa lazima kuna namna na si ndogo wallahi. Napendekeza, tusipinge tu. Mnaonaje tukaamua kwenda huko huko Ewuuura tukawape maazimio ambayo shurti leo tuyafikie na kupanga siku ya kuwapelekea?”

“Wazo lako la mbolea sana. Kama wanataka kutugeuza rubber stamp, acha tuwaendee huko huko. Tukifika tunahakikisha tunaandamana na waandishi wa habari ili warushe tendo hili takatifu na la ukombozi wa kaya. Tukishatoka huko, tunapeleka nakala ya maazimio yetu kwa rahis ili naye ajue tunavyopanga kuikomboa kaya yetu toka kwenye mikoni michafu ya majambazi wa kiuchumi wanaotaka kututumia kubariki ufuska wao; au vipi?” anachangia Mijjinga huku akibofya kisimu chake cha Sumsung 10.

Kanji anakwapua mic “veve dugu yangu asema jambo juri sana. Mimi iko nyuma yako na takwenda bele kama naamua kwenda toa hii azimio kwa wuura. Tena nakubali ile nasema kuva hii sasa natia vidole sisi. Kama nataka tenda haki kwanini nagoja muda refu sana? Kwanini napandisa bei ya umeme kila muaka nasi vachowu natobolewa kila siku?”

“Kanji hemu eeza vizuri tikueeewe. Natoboewa wapi na nani na kwanini? Na kwanini uwe nyuma yake ii ufanye nini? Nadhani hapa kia kitu chapaswa kuwa mbee kwa mbee.” Anajibu Mgoshi huku akimpa kikombe muuza kahawa ammwagie kahawa.

Kanji anacheka na kumtazama Mgoshi na kujibu “sasa kwanini tukana mimi. Kama veve hapana elewa ile nasema vatu vote kwanini nataka changia nini?”

Baada ya kuona utani unaanza kupoteza mada, Sofia Lion aka Kanungaembe anakatua mic “jamani acheni utani kwenye mambo nyeti. Nadhani alichomaanisha Kanji ni kuwa kaya yetu imekuwa ikichezewa na hawa wezi kiasi cha kugeuka shamba la bibi kama siyo kichwa cha chizi. Ni simpo hivi.”

Mheshimiwa Bwege aliyekuwa kimya muda mrefu anaamua kula mic “nataka niwe mkweli. Ninachoona hapa ni ukweli kuwa hawa jamaa kuwa wanaliwa kwa muda mrefu kwa kupewa vijisenti kidogo, wanataka na wananchi waingizwe kwenye ulaji huu wa kipuuzi. Nakubaliana na wanaohoji ni kwanini rahis Kanywaji ameshikwa na kigugumizi kuhusiana na kadhia hii ambayo iko wapi kuwa tunapigwa kiasi cha wachovu kulanguliwa umeme na kufanya maisha yawe aghali bila sababu tokana na ujambazi huu wa IpTL. Suluhu ya tatizo hili ni simpo. Kamata akina Rugemalayer, gabacholi Singasinga na akina Njaa Kaya na Ben Makapi walioingiza ujambazi huu wa nchana au vipi? Taifisha mali zote walizopata na kuwanyonga ili kupumzisha mzimu wa hujuma hii kwa kaya. Simpo.”

Kijiwe kikiwa ndiyo kinachanganya si lakapita shangingi la Rugemalayer! Kwa vile tulikuwa na usongo, tulinkamata na kumfanyia kitu mbaya ambacho si vizuri kutaja hapa tokana na kuheshimu maadili. Hata hivyo, “mimba” yake karibuni itazaliwa ili kuwa mwanzo wa mwisho wa kashfa ya ufuska wa IpTL.

Chanzo: Tanzania Daima Jumatano kesho

Tuesday, 13 June 2017

 

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s