Mlevi kutia timu Ukanadani kudai njuluku

        Baada ya wanene kutupiga changa la macho kuwa wale waliowaita majizi sasa ni “wanaume” kama alivyokaririwa dingi akisema, nimeamua kutia timu Ukanadani kudai changu. Yule anatikisa kichwa; akidhani natania. Sitanii. Lazima nifanye kweli hasa baada ya kuona kama tunapikiwea zengwe.
        Wanaodhani ulevi na ulimbukeni vinanisumbua kama wale waliogeuza kaya ya walevi shamba la bibi halafu sasa wanatwambia kuwa tuwasulubu makuwadi wao wenyewe wakikingiana vifua utadhani kaya yetu ni mali ya kaisari pekee yake wanakosea. Nitafanya kweli.
        Zifuatazo ndizo sababu za nguvu zinazonisukuma kulianzisha ili nipate changu mapema usawa huu wa Chukua Chako Mapema:
       Mosi, nimeamua kudai changu baada ya kupata ushahidi kwa dingi mwenyewe kuwa kumbe wale tuliaminishwa na bingwa wa uvivu wa kufikiri Brother Denjaman Tunituni ni wawekezaji kumbe wachukuaji na wezi wa kawaida wanaopaswa kuchomwa moto na si kujadiliana nao. Hivyo, lazima niwabane wanipe changu mapema kabla sijamnyotoa mwizi roho. Wakikomaa nawapeleka kwa pilato tena kule ICC ambapo nitafungua mashitaka ya mauaji ya halaiki ya walevi kwenye migodi kule Bulyankulu na North Mara ukiachia mbali wanaofishwa na umaskini wa kutengenezwa. Nina ushahidi kibao; wachukuaji hawa wezi walinyotoa roho za walevi.
        Pili, nimestuka kusikia kuwa jamaa sasa wamegeuka washirika na washikaji tena wakipongezana kuwa ni wanaume kiasi cha kuanza mikakati ya kujadiliana ili kulipana. Tangu lini mwenye mali akajadiliana na mijizi? Mbona vibaka hamjadili nao zaidi ya kuwachoma moto; au ni kwa vile kuna wanene nyuma ya jinai hii? Hivi nani alituroga waswahili kiasi cha kuwashobokea watasha; na kusahau; hawa jamaa wana mizungu; na wamekuwa wakitukwamisha kiuchumi halafu wakitutukana kuwa sisi ni hamnazo na maskini wa kujitakia. Acheni uvivu wa kufikiri. Badilini sheria kabla ya kuingia kwenye mazungumzo. Mnakwenda kule na sheria zipi wakati zilizopo zinaruhusu upigaji?  Kama hamjui basi jueni. Kinachotaka kufanywa ni ukoloni wa kujitakia. Mtajuta halafu muanze kuja na rongorongo nyingine.
        Tatu, nimeamua kuchukua hatua hii adhimu baada ya kugundua kuwa lile zoezi la kubadili sheria za kijambazi za kaya ili kuziba mianya yote ya uchukuaji na umakinikia sasa limeota mbawa baada ya kuja na sinema hii ya majadiliano. Lazima niseme wazi. Nitakuwa na uhakika gani kuwa wale watakaoshiriki haya majadiliano hawatakuwa na roho mtakakitu kama wale mbweha waliouza kaya yetu kwa wachukuaji kiasi cha kugeuka ombaomba wakati tuna raslimali kibao? Naweza kusema huu ni ubaguzi wa rangi. Hivi hii jinai ingekuwa ingetendwa na mswahili mweusi kungekuwa na cha kuongea au kufunga maisha? Hivi kweli nani alituroga kiasi cha kuwa kama ndondocha huku tukifanya mchezo na mambo muhimu ukiachia mambo ya hovyo kuyageuza ya maana kana kwamba hatuna maana? Hivi huu ujambazi ungekuwa umetendwa na kaya ya Kiswahili dhidi ya kaya ya kitasha unadhani kungekuwa na majadiliano? Kawaulize Wairaki na walibywa watakwambia jamaa hawa wasivyo na mchezo na kaya uchwara ombaomba kama zetu.
         Tano, baada ya kugundua kuwa mambo yenyewe sasa yatafanywa kwa kutegemea usongo wa dingi na si sheria kiasi cha kugeuka kama mali binafsi, nami sina budi kuanza madai binafsi. Hapa lazima nikomae na kuwa makini na si makinikia. Lazima nidai hata njuluku za madini na si makinikia yaliyogawiwa na majambazi wakubwa wasio na umakini bali umakinikia kiakili. Naona yule anasonya. Atakayechukia uje yumo. Kwani hawa waliogawa madini yetu walitumia nini zaidi ya makinikia ya akili badala ya akili yenyewe? Kama si hivyo, inakuwaje tushupalie makinikia huku tukifumbia macho madini yenyewe? Kama siyo hivyo, inakuwaje tutegemee usongo wa mtu mmoja badala ya sheria na mkakati wa kaya kwa ujumla?
        Sita, napanga nikipewa changu najea kaya kuanza kudai mchakato wa katiba mpya. Kwa vile nitakuwa na njuluku kibao, nitazitumia kuwahamasisha walevi kuhakikisha katiba mpya inapatikana ili iweze kutusaidia kupambana na mibaka yote iliyohusika na uchafu huu bila huruma wala upendeleo kama ilivyo. Hapa lazima nihakikishe natumia njuluku yangu kuanzisha kile kinachoitwa haki sawa kwa walevi wote bila kujali sura, vyeo, ubashite na upuuzi mwingine ninaoona kila siku kilevi kayani. Bila shaka hapa walevi watanipongeza kwa kila hatua badala ya kupongeza wale wale walioasisi ujambazi huu.
        Kumbe nafasi imeisha! Acha nijikate kwenda kutafuta pasipoti tayari kwa kuwatokea wamakinikia kwa umakini.
Chanzo: Nipashe Jumamosi leo.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s