Tag: july

Wizi wa Escrow tuanze na IPTK

            Hakuna utata; kampuni la the Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ni donda ndugu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa. Sitapenda kuongelea kesi iliyofunguliwa hivi karibuni dhidi ya watuhumiwa wa shilingi zipatazo bilioni 300 toka mfuko wa Escrow kwa vile iko mahakamani. Badala yake nitajadili namna ya kupambana na wizi huu ili taifa lisipate hasara tena.
            Kwa wanaojua namna kampuni tatanishi la IPTL lilivyoingizwa nchini kinyemela chini ya utawala wa awamu ya pili baada ya taifa kukumbwa na uhaba wa umeme kwenye miaka ya 90, watakubaliana nami kuwa ndilo chimbuko la wizi wa Escrow na hujuma nyingine ambazo zimekuwa zikiendelea dhidi ya taifa kwa zaidi ya miaka 20 hasa ikizingatiwa kuwa nusu ya wamiliki wake ndiyo wako mahakamani kwa tuhuma za wizi huu.
            IPTL ikiwa imeingizwa nchini na watawala wezi, ilianza kuhujumu taifa na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kiasi cha kuliua na kulifilisi hadi serikali ikawa inalikwamua huku wahujumu hawa wa uchumi wakiendelea kushika kani katika kuliibia na kulihujumu taifa. Pia, kutokana na hujuma hii, ambapo TANESCO iliuziwa umeme kwa bei mbaya, wateja wa nishati nchini walikuwa wakilanguliwa na kupandishiwa bei za umeme kila mara wakati taifa likiwa na vyanzo vingine imara kama vile maporomoko ya Stigler ambayo hivi karibuni rais John Magufuli alianza juhudi za maksudi kuyaendeleza ili taifa lijitosheleze kwa umeme na kuondoka kwenye mikono ya matapeli wa ndani nan je wanaotumia uhaba wa nishati kama mtaji na kijiko cha kutuhujumu na kutuibia. Baadhi ya vyanzo vyetu vinasema mradi huu ulizuiwa maksudi ili IPTL na makampuni mengine kama yale yaliyozaliwa na kashfa ya Richmond iliyozaa makampuni ya Dowan na Symbion kuendelea kuliibia na kulihujumu taifa. Nayo yanapaswa kushughulikiwa sambamba na IPTL. Kwani sifa na kazi zao ni moja tu, kuhujumu na kuliibia taifa.
            Kwanini tunasema kuwa bila kushughulika na IPTL mchezo utaendelea? Tuna sababu kuu zifuatazo:
Mosi, watuhumiwa wa kashfa ya Escrow walitumia IPTL hii hii pamoja na utata na kuisha muda wake kuliibia taifa. Inashangaza kwa kampuni ambalo limekuwa likihujumu taifa kuendelea kufanya biashara nchini ukiachia mbali kutochukuliwa kwa mali zake na uchafuzi wa mazingira ambao limekuwa likisababisha.
Pili, tunaambiwa IPTL inamilikiwa na watuhumiwa wawili kwa asilimia 50 ambapo asilimia zilizobaki zinamilikiwa na Simba Trust ambayo hata hivyo, tangu sakata hili lianze, huwa haitajwi hadharani. Je nani wamilki wa Simba Trust? Umma ungepaswa kuwajua ili nao waunganishwe kwenye kesi inayoendelea kwa vile isingewezekana wabia nusu wachukue mabilioni haya na wayatafune peke yake.
Tatu, kuna haja ya kutangazia watanzania kuwa IPTL haina uhalali tena wa kufanya biashara Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa–licha utata wa mkataba wake na kushiriki uhujumu wa taifa–muda wake ulikwisha siku nyingi. Hapa lazima tuseme wazi kuwa IPTL ina washitiri na washirika nchini tena wenye madaraka. Rejea hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) illivyotaka kuihalalisha IPTL kwa mara nyingine kwa kutaka watanzania wachangie maoni yao kabla ya kupewa leseni tofauti na makampuni mengine yanayofanya biashara nchini. Hivyo basi, serikali–licha ya kuwafichua Simba Trust–inapaswa kuwafichua maafisa wa umma na binafsi ambao wamekuwa wakiisaidia IPTL kuendelea kufanya biashara nchini kinyume cha sheria ukiachia mblai kuhujumu taifa. Haiingii akilini kuwa kampuni tapeli na la kigeni lingeweza kuendelea kuhujumu na kuibia taifa bila kuwa na watu wenye vifua serikalini na nchini kulikingia kifua. Mfano, wote walioshutumiwa kupokea mamilioni na mabilioni ya Escrow wanapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani huku mali zao zikikamatwa ili kurejesha fedha ya umma. Na hapa tusisikie kelele za mawakala na makuwadi wao kuwa tunawatisha wawekezaji.  Hawa si wawekezaji bali wachukuaji wanaopaswa kunyolewa bila maji wala huruma kama walivyokuwa wakilifanyia taifa.
Nne, kukata mzizi wa fitina, sheria za nishati zibadilishwe ili kuzuia mianya ambayo ilitumiwa na makapuni kama IPTL kuliingiza taifa kwenye mdororo na mgogoro wa kiuchumi tokana na ulafi, ujinga na ufisadi wa watu wachache wasioona mbali.
Tuhitimishe kwa kupongeza na kuunga mkono juhudi mahsusi na za maksudi anazofanya na serikali ya rais Magufuli kuliondoa taifa kwenye mikono ya matapeli na wezi wanaorejesha maendeleo ya taifa na watu wake nyuma. Tunashauri wahusika wapewe adhabu kali ili liwe somo kwa wengine wanaodhani Tanzania ni shamba la bibi. Yote yafanyike; ila muhimu, bila kusambaratisha IPTL, ni kama tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Kwani kuendelea kuwapo kwake na makampuni yanayofanana nayo si tishio tu kwa uchumi wa taifa bali hata usalama wake.
Kwa miongo tuliyotapeliwa, kuibiwa na kuhujumiwa, kama taifa lenye watu wenye akili, tufikie mahali tukate mizizi ya fitina mojawapo ikiwa ni kampuni ya IPTL.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili leo.