Tag: jumapili

Barua ya wazi kwa maaskofu Kilaini na Nzigilwa

Image result for photos of kilaini na nzigilwa
          Wahashamu maaskofu Methodius Kilaini na Eusebius Nzigilwa,
            Kwanza, nawaamkua shikamooni; na kukwapa pole kwa majukumu yetu ya kiroho na kidunia. Pia nawapa pole kwa yaliyowakuta. Maana si madogo. Ni pale mlipotuhumiwa, kabla ya kukiri, kuchotewa fedha zilizotokana na kashfa ya wizi wa fedha za umma wa watanzania maskini ijulikanayo kama Escrow mlizopewa na mtuhumiwa na muasisi mkuu wa kashfa hii, James Rugemalira ambaye sasa yuko korokoroni akituhumiwa kwa makosa ya kulihujumu taifa na kuuibia umma. Hivyo, sitaweza kuingi undani wa suala zima tokana na sababu za kisheria na ukweli kuwa mnalijua vizuri hata kuliko mimi kama wanufaika ambao sasa wanajitenga na mshitili wao.
            Hivi karibuni, nilisoma tangazo lenu la tarehe 7 Septemba, 2017 kuutaarifu umma kuwa mmeamua kurejesha zile fedha kwa serikali baada ya kujiridhisha kuwa hazikupatikana kihalali. Je mmetubia dhambi hii itokanayo na uroho ambayo ni kinyume cha mafundisho ya Yesu Kristo? Je mmetumia vigezo gani hasa ikizingatiwa kuwa atoaye sadaka kanisani au matoleo, kama manavyoita, huwa haulizwi namna alivyochuma fedha atoazo? Maana ingekuwa hivyo, bila shaka mngelimuuliza Rugemalira alivytengeneza hiyo fedha kabla ya kuzichukua na kuishia kwenye kashfa ambao itawagharimu vilivyo kama mkondo wa sheria utafuata ikizingatiwa nyinyi ni viongozi na watumishi wa umma waliopokea fedha chafu zitokanazo na wizi wa fedha za umma. Je huu si ushahidi tosha kuwa hii fedha haikuwa ya kanisa bali yenu kutokana na kitendo mlichofanya mkidhani kitawasafisha kikaishia kuwafichua na kuwachafua zaidi?  Katika tangazo tajwa hapo juu, mnakiri kupokea fedha ambazo hamkutaja ni kiasi gani ingawa inafahamika ni shiling milioni 40 na ushei, hapo Februari 2014 kupitia kwenye akaunti zenu za benki.  Hii maana yake ni kwamba fedha tajwa ilikuwa benki kwa takriban miaka mitatu ikitengeneza faida. Je mmerejesha na interests zilizolipwa na benki tokana na kuwa na kiasi hiki kikubwa? Je tukiacha ubabaishaji na kujitetea, kweli kwenye nafsi zenu hamkujua kuwa fedha hii ilikuwa kubwa; na uwezekano wa mhusika kuipata visivyo halali ulikuwa mkubwa ikizingatiwa kuwa kashfa yake haikuanza jana wala juzi? Je mnategemea kufanikisha nini katika hatua hii ambayo kisheria ni ushahidi wa wazi unaoweza kutumika dhidi yenu? Je kwanini mlingoja mpaka Rugemalira akamatwe? Je angeendelea kunyamaziwa mngechukua hatua mlizochukua au ni baada ya kugundua kuwa mambo sasa si mchezo wala mazoea kama ilivyokuwa imezoeleka nchini ambapo mafisadi wakubwa walizoea kulindwa na kuengwaengwa huku wakiwakoga wale waliowaibia? Kuna haja ya kutubu na kujisuta sana huku mkisema ukweli ili mueleweke na ikibidi kusamehewa au kuhukumiwa kulingana na wenye fedha watakavyoamua.
            Wapendwa, naomba niendelee kuwadodosa lau ukweli ujulikane ili uwaweke huru.  Katika tangazo lenu mlidai kuwa fedha husika ilikuwa ni matoleo.Je kama kweli yalikuwa ni matoleo, kwanini yaliingizwa kwenye akaunti zenu na si kwenye akaunti za makanisa yenu? Hapa nani anasema ukweli; na utaratibu wa kupokea matoleo ni upi kwa mujibu wa kanuni za kanisa? Je kwanini mmeamua kurejesha fedha serikalini na si kwa yule aliyewapa au familia yake wakati mkijua serikali aihusiki kwenye kashfa hii? Je mlipata ushauri wa kisheria ua wa kidini katika kufikia hatua hii hatari. Kwani, kiushahidi wa mazingira, hamna tofauti na wanufaika wengine waliohongwa tokana na nafasi zao katika utumishi wa umma ambao nanyi, kama watumishi wa kiroho, mnahusika? Je kitendo chenu cha kupokea fedha chafu kwenye akaunti binafsi kinatoa funzo na picha gani kwa jamii yetu? Je mnadhani mlichofanya ni suluhu ya sakati hili linalopaswa kuisha kisheria?
            Wapendwa, japo sitaki niseme mengi wala kuhukumu ili nisihukumiwe, tangazo lenu limeficha mengi zaidi ya liliyoweka wazi. Kwa mfano, kwanini hamkueleza utaratibu unaojulikana kikanisa wa muumini kutoa matoleo kwa kanisa ili umma upime kama kilichofanyika ni sawa au si sawa? Je kwanini mmechukua muda mrefu kufikia uamuzi mliofikia? Lazima kuwe na sababu zaidi ya mhusika kuwa korokoroni. Je mlifanya jitihada za kumrejeshea aliyewapa hiyo fedha kabla ya kufikia kuzipeleka serikali au mnafanya hivyo, ili serikali na umma usiwashughulikie?
            Nimalizie kwa kusema kuwa kitendo chenu kinaacha maswali mengi kuliko majibu. Sidhani kama serikali itaona sincerity kwenye kitendo hiki zaidi ya kuwa mbinu ya kutaka kuepukana na matokeo ya kashfa hii ambayo ni kufikishwa mbele ya vyombo vya dola ili haki itendeke. Maana, hali tuliyo nayo nchini kwenye ufisadi inatisha na kukatisha tamaa ingawa rais anajitahidi kupunguza madhara na ukubwa wa tatizo ambalo watangulizi wake walililea na kulifumbia macho. Si viongozi wa serikali wala wa kiroho japo si wote, imewaozesha na kuwaharibu kiasi cha kusahau hadhi, heshima na wajibu wao kwa umma. Ushauri wangu wa bure kwenu ni kwamba kirini kukwa mlipotoka na muombe msamaha mambo yaishe ili liwe somo kwa wengine wanaodhani kuwa wanaweza kutumia nyadhifa zao kula na mafisadi.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili leo.

Katiba mpya somo toka Kenya

Image result for photos of rasimu ya katiba mpya
          Japo wakenya wakisema kuna mambo wanazidi nchi nyingine huonekana kama wanajisifia sawa na watanzania. Mfano, wakenya huiita nchi yao economic hub of East and Central Africa sawa na watanzania wanavyojiita kisiwa cha amani barani Afrika. Kuna mambo wakenya wana haja ya kujisifia sawa na watanzania na wananchi wengine wa nchi za kiafrika zilizotengenezwa na mkoloni jambo ambalo linaonyesha namna tunavyoshangilia ukoloni kiasi cha kuushiriki kwa namna moja au nyingine.
            Pamoja na mijisifa mingine isiyo na msingi, kwa sasa Kenya inangia kwenye kundi teule barani la nchi za Afrika ya Kusini, Botswana na Ghana kama nchi zinazoweza kujisifu kuwa zina katiba zilizostaarabika. Kwani, katiba za nchi hizi zimefanya kila mhimili wa dola kujitegemea na kutoingiliwa wala kuingilia mihimili mingine kama inavyotaka dhana ya utawala bora na wa sheria. Chini ya dhana hii, juzi dunia, kwa mara ya kwanza, ilishuhudia ushindi wa rais ukifutiliwa na kubatilishiwa mbali na mahakama. Kitendo hiki, licha ya kuiletea Kenya sifa kedekede, kimeiweka mbele hata kuliko nchi vigogo vinavyojigamba kuwa mabingwa na walimu wa demokrasia kwa Afrika kama vile Marekani ambayo ina migogoro ya matokeo ya uchaguzi sawa na nchi za kiafrika.
            Pia uamuzi huu umekuwa suto karibu kwa nchi zote za kiafrika ukiondoa zile zilizoonyeshwa hapo juu. Ni suto sana kwa Afrika Mashariki ambayo licha ya kuwa na serikali mbili tu za kidemokrasia za Kenya na Tanzania, ina wingi wa viongozi ving’ang’anizi wa madaraa chini ya visingizio mbali mbali.
            Leo safu hii itaangalia masomo yanayopatikana kwenye uamuzi wa mahakama kuu ya Kenya wa kufutilia mbali ushindi wa rais. Kwanza, haijawahi kutokea popote duniani. Je Kenya imefanya hivi kutokana na kuwa na watu wa ajabu? Hasha. Ni kutokana na kuwa na katiba bora yenye kutokana na utashi na mawazo ya wananchi iliyoanza kutumika mwaka 2010. Katiba ya Kenya inatoa haki kwa raia yoyote kupinga matokeo yoyote katika nafasi za kuchaguliwa hata kuteuliwa anapohisi haki haikutendeka. Wakati Katiba ya Kenya ikifanya hivyo, ya Tanzania hairuhusu hata kuhoji matokeo hasa ya urais. Inamuweka rais juu ya sheria jambo ambalo licha ya kuwa moja ya masalia ya ukoloni, ni aina fulani ya ukoloni ulioendelezwa na watawala waliopokea uhuru na waliowafuata kwa hofu ya kuondolewa madarakani hata kushitakiwa walipovurunda.
            Pili, tokana na kuwa na Katiba inayotoa uhuru na haki kwa wananchi wengi, hata taasisi za Kenya kama vile Mahakama  na nyingine zinao uhuru na wajibu kwa wananchi wote bila kujali mamlaka yao. Hivyo, mahakama ya Kenya ni huru; na uamuzi wake hauwezi kuingiliwa na mhimili mwingine kama ilivyo kwenye nchi nyingine ambako mahakama hutumika kama mhuri au rubberstamp wa utawala.
            Si mahakama tu. Hata bunge la Kenya lina haki na uhuru kuliko mabunge mengi ya Afrika ambayo hutumika kama nyumba ndogo za utawala katika kulinda na kuendeleza uovu. Mifano midogo ni nchini Rwanda na Uganda ambapo mabunge yalipitisha sheria za kuruhusu watawala wao kubadilisha katiba ili kubakia madarakani kinyume cha matakwa ya wananchi.
            Tukija Tanzania, bunge letu bado si huru tokana na kuwa na wabunge wengi wa chama tawala; jambo ambalo hulifanya lipitishe mambo ya hovyo bila kuogopa kushughulikiwa kisheria. Ukiachia hili, ukosefu wa sheria inayolipa madaraka hata likiwa chini ya chama kimoja kama mhimili wa dola yanaonekana namna chama tawala kinavyolitumia litakavyo bunge. Mfano wa hivi karibuni ulijitokeza hivi karibuni nchini Afrika Kusini ambapo katiba huru hulipa bunge uhuru. Baada ya vyama vya upinzani kutoridhishwa na udhu wa rais wa nchi hiyo mwenye wingi wa kashfa za rushwa na ukosefu wa maadili hata binafsi Jacob Zuma, walikwenda mahakamani  na bunge likaamuru rais apigiwe kura ya kutokuwa naye imani. Kama si kuwa na wabunge wengi wa chama chake–ambacho kimechakaa tangu aondoke rais wa kwanza wa nchi hiyo shujaa Nelson Mandela kama CCM baada ya Nyerere– walimuokoa. Ingekuwa Tanzania nani alitegemea upinzani upeleke hoja bungeni halafu spika aipitishe? Ni mara moja ilipotokea bunge likapitisha hoja ya kutaka kuishughulikia serikali mwaka 2008 ambapo–tokana na siasa za makundi ndani ya chama tawala na ushiriki wa rais mwenyewe kwenye kashfa–alimtoa kafara waziri wake mkuu.
            Somo jingine linalotolewa na ubatilishwaji wa matokeo ya urais nchini Kenya ni kwamba Tanzania inahitaji kufikiri upya juu ya kuendelea kuua rasimu ya katiba mpya ya wanachi iliyolenga kuondoa mabaki ya ukoloni Tanzania ambayo imekuwa ikiendeshwa na katiba viraka ya zamani isiyo endana wala kukidhi matakwa ya watanzania. Katiba ya sasa ni ya watawala na si ya wananchi tofauti na katiba ya Kenya ambayo ni ya wananchi na wanaweza kuitumia dhidi ya watawala hata akiwamo rais bila kikwazo wala woga.
            Tumalizie kwa kuwataka watanzania na  hata watawala kuanzisha mchakato wa kudai kurejeshwa kwa mchakato wa katiba mpya kama kweli si wanafiki wanataka kuikomboa na kuiendeleza nchi kama wengi wanavyosema. Tunataka matendo na si maneno. Tunataka katiba mpya sasa.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili kesho. Saturday, 2 September 2017

Kumpinga rais au serikali si jinai

Sunday, 9 July 2017

            Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari viliingia utatani hadi vingine kufungiwa huku wanasiasa na wakosoaji wakipewa onyo kali kuacha ima kuipinga serikali au rais. Tukio la hivi karibuni ni pale rais John Pombe Magufuli alipoamuru polisi kuwakamata wote wanaohoji baadhi ya mambo anayofanya kama vile kushindwa kudhibitiwa kwa mauaji ya Kibiti, upelekaji bungeni mikataba ya haraka bungeni, hata baadhi ya hatua anazochukua kuhusiana na mambo mbali mbali kama vile uhuru wa vyama vya siasa kufanya siasa.
            Tokana na utata huu–ambao wengine huuona kama uimla–kuna haja, kama taifa, kukaa pamoja na kukubaliana namna ya kuendesha nchi yetu hasa vita dhidi ya uhujumu wa taifa na tishio dhidi ya usalama wa raia. Hivyo basi, leo nitadurusu mambo muhimu ambayo pande zote zinapaswa kuzingatia kama ifuatavyo:
Mosi, Tanzania si mali ya rais, serikali wala chama tawala. Ni mali ya watanzania wote kwa usawa. Hivyo, kila mtanzania ana uwezo wa kuamini aonavyo ilmradi asivunje sheria. Kwani, kwa mfano, wanaohoji mambo hayo hapo juu, hawatendi kosa lolote hasa ikizingatiwa kuwa kila binadamu amejaliwa uhuru na uwezo tofauti wa kuyadurusu na kuyaelewa mambo.  Hivyo, kutishiana kukamatwa na polisi si jibu wala njia sahahi kwa mustakabali wa taifa letu. Tupingane kwa hoja na si vitisho wala kutumia misuli ya dola. Baba wa taifa Mwl Julius Nyerere alituachia tunu tatu kuu. Moja uvumilivu, pili, kujibu hoja kwa hoja kwa njia ya majadiliano, na tatu uadilifu. Kimsingi, uadilifu ni sehemu mojawapo ya kuwathamini wengine na michango yao na si juu ya mali wala fedha tu.
            Pili, matumizi ya vyombo vya dola kunyamazisha wakosoaji ni uvunjaji demokrasia jambo ambalo ni jinai bila kujali anayelitenda ni nani au ana cheo gani. Kwani, kama nilivyoeleza hapo juu, kila binadamu amepewa ubongo afikiri atakavyo na kuhoji na kujibu anachojua au kutilia shaka. Hapa lazima tuelewe; kama mtu anasema uzushi, tunampa ukweli lakini si kumnayamazisha. Tunaweza kuwafunga wakosoaji hata magezeti lakini hatuwezi kufunga akili na vinywa vyao.
            Tatu, kwani rais na serikali yake hawakosei? Rais ni binadamu na serikali yake inaendeshwa na binadamu. Sijui, kwa mfano, serikali inapata wapi jeuri ya kutaka kuwanyamazisha wapinzani wanaohoji miswaada ya sheria chini ya hati ya dharura bungeni wakati ni miswaada na staili hiyo hiyo iliyosababisha kutungwa sheria mbaya za kifisadi hadi Tanzania ikawa inaibiwa mchana kweupe? Je ni serikali ya chama gani iliyoingia upuuzi huu kama siyo hii hii iliyoko madarakani? Hivi kuhoji huyu roho mtakatifu alipotekea nalo ni kosa au tunapenda kurudia makosa tu bila sababu? Nani amesahau wabunge kama David Kafulila, John Mnyina na Zitto Kabwe hata walivyofurushwa bungeni kwa kupinga sheria mbovu zinazobadilishwa kwa sasa? Hawa nao wanyamaze wakijua wazi kitakachotokea baada ya kufanya mambo kwa kukurupuka? Kama tumeibiwa miaka 20 tukavumilia–japo si jambo jema–inakuwaje tukurupuke kama tulivyokurupushwa na waliobariki huu ufisadi? Nadhani shughuli za taifa si za kuaminiana tu bali kutiliana shaka na kuchunguzana. Na isitoshe, hizi siyo zama za chama kimoja na zidumu fikra za mwenyekiti.
            Nne, kama wabunge wanaowawakilisha waliowachagua kufanya hivyo wametumwa kusema wanayosema, inakuwaje mnawatisha na kuwafukuza kama mtu mmoja wakati wanawakilisha wale waliowatuma? Sasa nini faida ya kuwa na wabunge kama wabunge wote wanapaswa kuwa ndiyo mzee? Naungana na baadhi ya wabunge waliosema kuwa badala ya kuwatisha na kuwaona kama maadui wa taifa, basi tubadili katiba na kuendesha nchi kwa chama kimoja bila kujali kuwa kile kilichotufanya tutoke huko bado kiko pale pale au tunataka tuendelee kulazimishwa na wazungu namna ya kuendesha nchi yetu kutokana na kutokubaliana na baadhi ya mambo? Mfano, nani amempa rais mamlaka ya kujadiliana na kampuni ya Barrick huku vyombo vya dola vikiigwaya kampuni inayotuhumiwa ya Acacia? Je hili pekee halionyeshi kuwa tunaanza vibaya kumdai mtu ambaye huna mkataba naye eti kwa vile ni mbia wa aliyekuibia? Ni sheria na busara gani hii jamani?
            Kwa waliosoma Migogoro na utatuzi wa migogoro (Conflict Resolution Studies) wanajua fika kuwa katika mgogoro wowote lazima kuwapo na watu au makundi zaidi ya moja yanayogombea hiki moja au parties to conflict. Hawa wanaweza kujiwakilisha kwenye majadiliano na wataalamu wa eneo husika lakini hawawezi kujivua uhusika. Mfano, ukiwa na ugomvi nami, siwezi kuwakilishwa na mke wangu kama party to conflict vinginevyo aje kama mtaalamu au mteuliwa tu asiye na uwajibikaji kisheria bali kukusemea tu.
            Tumalizie kwa kuitaka serikali itambue kuwa hata wanaoipinga, licha ya kuwa na haki kufanya hivyo, wana akili sawa na hawa wanaowapinga. Pia wafahamu na kukubali kuwa wanapingwa tokana na historia yao yaani kuingia mikitaba mibovu. Na mwisho, wao si Mungu asiyekosea; ni wanadamu tu wa kawaida. Wangekuwa hawakosei wala wasingekosea kwa madudu yanayotuhangaisha kama taifa.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili leo.

Wizi wa Escrow tuanze na IPTK

            Hakuna utata; kampuni la the Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ni donda ndugu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa. Sitapenda kuongelea kesi iliyofunguliwa hivi karibuni dhidi ya watuhumiwa wa shilingi zipatazo bilioni 300 toka mfuko wa Escrow kwa vile iko mahakamani. Badala yake nitajadili namna ya kupambana na wizi huu ili taifa lisipate hasara tena.
            Kwa wanaojua namna kampuni tatanishi la IPTL lilivyoingizwa nchini kinyemela chini ya utawala wa awamu ya pili baada ya taifa kukumbwa na uhaba wa umeme kwenye miaka ya 90, watakubaliana nami kuwa ndilo chimbuko la wizi wa Escrow na hujuma nyingine ambazo zimekuwa zikiendelea dhidi ya taifa kwa zaidi ya miaka 20 hasa ikizingatiwa kuwa nusu ya wamiliki wake ndiyo wako mahakamani kwa tuhuma za wizi huu.
            IPTL ikiwa imeingizwa nchini na watawala wezi, ilianza kuhujumu taifa na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kiasi cha kuliua na kulifilisi hadi serikali ikawa inalikwamua huku wahujumu hawa wa uchumi wakiendelea kushika kani katika kuliibia na kulihujumu taifa. Pia, kutokana na hujuma hii, ambapo TANESCO iliuziwa umeme kwa bei mbaya, wateja wa nishati nchini walikuwa wakilanguliwa na kupandishiwa bei za umeme kila mara wakati taifa likiwa na vyanzo vingine imara kama vile maporomoko ya Stigler ambayo hivi karibuni rais John Magufuli alianza juhudi za maksudi kuyaendeleza ili taifa lijitosheleze kwa umeme na kuondoka kwenye mikono ya matapeli wa ndani nan je wanaotumia uhaba wa nishati kama mtaji na kijiko cha kutuhujumu na kutuibia. Baadhi ya vyanzo vyetu vinasema mradi huu ulizuiwa maksudi ili IPTL na makampuni mengine kama yale yaliyozaliwa na kashfa ya Richmond iliyozaa makampuni ya Dowan na Symbion kuendelea kuliibia na kulihujumu taifa. Nayo yanapaswa kushughulikiwa sambamba na IPTL. Kwani sifa na kazi zao ni moja tu, kuhujumu na kuliibia taifa.
            Kwanini tunasema kuwa bila kushughulika na IPTL mchezo utaendelea? Tuna sababu kuu zifuatazo:
Mosi, watuhumiwa wa kashfa ya Escrow walitumia IPTL hii hii pamoja na utata na kuisha muda wake kuliibia taifa. Inashangaza kwa kampuni ambalo limekuwa likihujumu taifa kuendelea kufanya biashara nchini ukiachia mbali kutochukuliwa kwa mali zake na uchafuzi wa mazingira ambao limekuwa likisababisha.
Pili, tunaambiwa IPTL inamilikiwa na watuhumiwa wawili kwa asilimia 50 ambapo asilimia zilizobaki zinamilikiwa na Simba Trust ambayo hata hivyo, tangu sakata hili lianze, huwa haitajwi hadharani. Je nani wamilki wa Simba Trust? Umma ungepaswa kuwajua ili nao waunganishwe kwenye kesi inayoendelea kwa vile isingewezekana wabia nusu wachukue mabilioni haya na wayatafune peke yake.
Tatu, kuna haja ya kutangazia watanzania kuwa IPTL haina uhalali tena wa kufanya biashara Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa–licha utata wa mkataba wake na kushiriki uhujumu wa taifa–muda wake ulikwisha siku nyingi. Hapa lazima tuseme wazi kuwa IPTL ina washitiri na washirika nchini tena wenye madaraka. Rejea hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) illivyotaka kuihalalisha IPTL kwa mara nyingine kwa kutaka watanzania wachangie maoni yao kabla ya kupewa leseni tofauti na makampuni mengine yanayofanya biashara nchini. Hivyo basi, serikali–licha ya kuwafichua Simba Trust–inapaswa kuwafichua maafisa wa umma na binafsi ambao wamekuwa wakiisaidia IPTL kuendelea kufanya biashara nchini kinyume cha sheria ukiachia mblai kuhujumu taifa. Haiingii akilini kuwa kampuni tapeli na la kigeni lingeweza kuendelea kuhujumu na kuibia taifa bila kuwa na watu wenye vifua serikalini na nchini kulikingia kifua. Mfano, wote walioshutumiwa kupokea mamilioni na mabilioni ya Escrow wanapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani huku mali zao zikikamatwa ili kurejesha fedha ya umma. Na hapa tusisikie kelele za mawakala na makuwadi wao kuwa tunawatisha wawekezaji.  Hawa si wawekezaji bali wachukuaji wanaopaswa kunyolewa bila maji wala huruma kama walivyokuwa wakilifanyia taifa.
Nne, kukata mzizi wa fitina, sheria za nishati zibadilishwe ili kuzuia mianya ambayo ilitumiwa na makapuni kama IPTL kuliingiza taifa kwenye mdororo na mgogoro wa kiuchumi tokana na ulafi, ujinga na ufisadi wa watu wachache wasioona mbali.
Tuhitimishe kwa kupongeza na kuunga mkono juhudi mahsusi na za maksudi anazofanya na serikali ya rais Magufuli kuliondoa taifa kwenye mikono ya matapeli na wezi wanaorejesha maendeleo ya taifa na watu wake nyuma. Tunashauri wahusika wapewe adhabu kali ili liwe somo kwa wengine wanaodhani Tanzania ni shamba la bibi. Yote yafanyike; ila muhimu, bila kusambaratisha IPTL, ni kama tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Kwani kuendelea kuwapo kwake na makampuni yanayofanana nayo si tishio tu kwa uchumi wa taifa bali hata usalama wake.
Kwa miongo tuliyotapeliwa, kuibiwa na kuhujumiwa, kama taifa lenye watu wenye akili, tufikie mahali tukate mizizi ya fitina mojawapo ikiwa ni kampuni ya IPTL.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili leo.

Uhuru wa habari: Mbona viongozi wetu wanapingana?

        Katika kuangalia haki na uhuru wa kukusanya, kusambaza, kutoa na kupata habari nchini, leo nitajikita kuonyesha mkanganyiko uliopo serikalini kiasi cha kugeuka tatizo kubwa kwa baadhi ya vyombo vya habari visivyokuwa “ndiyo mzee.” Kufungiwa gazeti la Mawio hivi karibuni kutatumika kama kigezo cha kudurusu hoja hii.  Katiba ya Tanzania inampa uhuru kila mtanzania kutoa, kupokea, kusambaza, na kupata habari ilmradi asivunje sheria. Gazeti la Mawio lilifungiwa kwa miaka miwili. Kosa? Kuchapisha picha za marais wa zamani wanaohusishwa na ufisadi. Chanzo cha habari? Wabunge waliosema wazi kuwa marais wa zamani walioshiriki ufisadi–kubwa likiwa ni kuingia mikataba ya kijambazi–washitakiwe. Je hapa kosa la gazeti liko wapi; kuripoti kilichotamkwa hadharani tena mbele ya kamera na vinasa sauti vya vyombo vya habari? Wengi walidhani kuwa gazeti lilikuwa limeandika uzushi. Je si kweli kuwa, mfano, rais Benjamin Mkapa alijitwalia mgodi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira chini ya kampuni yake na mkewe iitwayo ANBEN yaani Anna and Ben ambayo ni majina ya kwanza ya Mkapa na mkewe?
            Wa pili kuhusishwa ni rais mstaafu Jakaya Kikwete. Je gazeti liliandika uzushi? Kama ni kukamata basi angekamatwa mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) Tundu Lissu aliyeliambia bunge kuwa mikataba ya hovyo ya uwekezaji kwenye madini–uliogeuka uchukuaji hata wizi kama alivyosema rais John Magufuli–ilisaniwa na Kikwete hapo tarehe 5 Agosti, 1994. Je si kweli kuwa Kikwete alisaini mkataba unaomhangaisha Magufuli na watanzania kwa ujumla? Kosa liko wapi hapa? Je na Lissu atafukuzwa bungeni? Nadhani wapinzani wameonyesha uzalendo wa hali ya juu kwa kuliita koleo koleo na si kijiko kikubwa; na kumkosoa rais au serikali si kosa kisheria.
            Sasa ngoja tuonyeshe serikali inavyojikanganya kiasi cha kujipinga na kuzua mkanganyiko. Hivi karibuni mkurugenzi wa Maelezo Dk Hassan Abbas alisema kuwa vyombo vya habari vinaruhusiwa kuikosoa serikali. Abbas alisema “hakuna chombo cha habari kitakachochukuliwa hatua kwa kukosoa, haki hiyo ipo kwa mujibu wa Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 kifungu cha 51, tutaendelea kuthamini na kufanyia kazi ukosoaji huo.” Je Mawio nalo limo humu; nalo si chombo cha habari?
            Bahati mbaya, hakutofautisha kati ya kuikosoa serikali na kumkosoa rais ambaye kimsingi ndiye mkuu wa serikali. Je kweli serikali haikosolewi? Mbona bosi wake anasema vinginevyo? Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Nape Nnauye aliyemteua Abbas kabla ya kutenguliwa uteuzi wake kwa kuwashika pabaya wasioguswa alikaririwa kabla ya kufukuzwa akisema “serikali ni rahisi sana kujisahau, ama inaweza ikaziba masikio, hivyo ni lazima pawepo na ‘very strong media’ zitakazofanya kazi ya kuiambia Serikali.” Je serikali haikujisahau kiasi cha kuingia mikataba ya kijinga? Strong media zinafungiwa; zinaachwa zinazojikomba. Huku ni kujipinga Dhahiri.
            Hata hivyo, kupingana kwa mteule na bosi wake hakuashii kwa Abbas.  Hata Nape anaonekana kupingana na aliyemteua yaani rais Magufuli ambaye alikaririwa akisema “nawaambia wamiliki wa vyombo vya habari be careful and watch it (kuweni waangalifu) kama mnadhani mna freedom (uhuru) ya namna hiyo not to that extent (siyo kwa kiasi hicho).” Kama haitoshi, Magufuli aliongeza kusema kuwa“uzalendo umepotea na unapotezwa na viongozi kwa interest (interests) (manufaa) zetu.” Kwanza, kwanini uzalendo uwe wa upande mmoja? Strong media hazijikombi; zinakosoa hata kama kufanya hivyo kunawaudhi wahusika. Bahati nzuri Magufuli anajua lilipo tatizo ila hataki kulishughulikia vilivyo.
            Mfano, Magufuli anasema “watoaji haki katangulizeni Tanzania, majaji mnafanya kazi nzuri katika kutafuta haki, tutengeneze Tanzania yetu, mimi nipo hapa temporary (kwa muda mfupi), makamu wa rais yupo temporary; everybody is (in power) temporary because the life is so temporary (temporal) (kila mtu yupo kwa muda mfupi kwa sababu maisha ni mafupi), lakini Tanzania yetu si temporary, itaendelea kuwepo tuilinde hii Tanzania yetu ambayo because it is suppose to (supposed to be) be there permanently (kwa sababu idumu).” Hii kidogo inashangaza. Mbona magufuli hatangulizi uzalendo kwa kukubali; Tanzania ni ya wote na wana mawazo hata kama ni kinzani? Kuna haja ya washauri wa rais kujitahidi kumkumbushwa anayosema ili asijipinge au kupingana na watendaji wake ukiachia mbali kuvunja sheria. Au Magufuli anafanya kile ambacho waingereza huita holier than thou kwa kutotaka kukosolewa wala kushughulikiwa watangulizi wake waliotenda uovu wa wazi bila sababu ya msingi zaidi ya tamaa na uroho wa kawaida?
            Tumalizie kwa kuwashauri washauri wa rais wawe wanamshauri vizuri kuhusiana na kupingana kwa serikali yake. Anaongelea uzalendo wakati akijua kuwa ni serikali za chama chake zilizoukosa na kuliingiza taifa kwenye matatizo ya ufisadi tunayopambana nao. Hata hivyo, nimshukuru Magufuli kwa kuanza kushughulikia kashfa makaburi kama vile Escrow. Ila asiume upande mmoja na kupuliza mwingine. Atende haki kimsumeno; akate mbele na nyuma bila kupatiliza wala kupendelea. Tanzania ni yetu sote bila kujali cheo cha mtu.  Kama serikali haitaki kukosolewa isikosee. Kama ikitaka kuheshimika ifanye mambo ya heshima; si ya hovyo kama kuingia mikataba ya hovyo. Tukiendelea kutishana, kupatilizana, kudanganyana, na kuogopana, kama taifa, tutaangamia. Hakuna asiyekosea.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili kesho.

Bila katiba mpya Magufuli anajipiga mtama

            Kupiga mtama ni neno la mtaani lenye kumaanisha kupiga ngwara. Kwa kishona humaanisha ujuzi au maarifa na maumivu ayapatayo mtu kidoleni hasa unapojikwaa. Leo nitatumia neno ngwara kuonyesha namna Tanzania, kwanza, ilivyohujumiwa kiasi cha rais John Magufuli kuuliza”nani alituroga Tanzania?”
        Nitajaribu kudurusu mambo au sababu zinazoikwamisha Tanzania au tuseme uchawi –kwa wale wanaoamini katika kurogwa kiasi cha kutaka kuombewa badala ya kuambiwa ukweli kuwa sisi ni sehemu ya tatizo. Hivyo natoa yafuatayo:
         Mosi, urathi wa au mabaki ya ukoloni au colonial carryover. Baada ya kupata uhuru na kurithi mfumo mbovu wa uongozi wa ima kuiga au kudandia, tulijikuta tukijenga matabaka ya watu miongoni mwa raia wetu. Hii unaweza kuiona kwenye sheria zinazoongoza nchi yetu kuhusiana na makosa ya wizi mkubwa na mdogo. Mtu akiiba kuku anafungwa miaka mingi kuliko anayeiba mabilioni. Wakoloni waliweka mfumo huu ili kuwafunga waswahili pale wanapowadokolea huku wakiwalinda mawakala wao ambao walikuwa wakinyanya fedha nyingi jambo ambalo tuliliendeleza hadi leo.
        Pili, ni ile hali ya nchi kuendesha na katiba zisizotokana na matakwa wala utashi wa wananchi au superimposed constitution. Katiba ya Tanzania haijawahi kutokana na wananchi. Badala yake ima ilitokana na mkoloni–baada ya majadiliano katika jumba la Lancaster–au chama kimoja–katiba ya jamhuri ya muungano ya mwaka 1977 iliyotokana na vyama vya Tanu na ASP. Kihistoria Tanzania imekuwa na katiba tano, yaani Katiba ya Uhuru (1961-62), Katiba ya Madaraka au Jamhuri (1962-64), Katiba ya Muda ya Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar (1964-77) na Katiba ya Jamhuri ya Muungano 1977 ambayo iliundwa baada ya vyama vya ASP na TANU kuunganishwa na kuunda Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo imekuwa ikifanyiwa marekebisho na kujaa viraka kiasi cha kujitenga na wakati na matakwa ya watanzania.
          Matumizi mabaya ya madaraka ya baadhi ya viongozi wetu. Rais wa Tanzania yupo juu ya katiba. Unategemea nini unapomuweka binadamu juu ya sheria zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka. Anayebishia hili arejee historia ya Tanzania aone namna serikali za kuanzia awamu ya pili hadi ya nne zilivyoshiriki na kuhalalisha ufisadi kiasi cha kuzaa kadhia ya ufisadi wa kutisha kama unavyoendelea kuibuliwa na serikali ya awamu ya tano. Tokana na rais kuwa juu ya sheria, karibu awamu zote tajwa zilitegemea utashi wa rais kuendeshwa. Mfano, rais wa awamu ya pili Ali Hassan Mwinyi aliporuhusu kile kilichotafsiriwa kuwa RUKSA, wengi hawakujua madhara yake. Kimsingi, hapa ndipo mizizi mikubwa ya ufisadi ilipojikita nchini. Haina maana kuwa hapa mwanzo hapakuwapo na rushwa. Ilikuwapo; ila mwalimu Julius Nyerere alijitahidi sana kupambana nayo chini ya mfumo wa Kijamaa ambao ulimpa uwezo wa kumwajibisha yeyote aliyeshuku alikuwa fisadi.
        Alipoingia Benjamin Mkapa–hasa muhula wake wa mwisho–viwango vya ufisadi vilikua zaidi hasa ilipobainika kuwa kumbe kuna watu waliomtumia yeye au mkewe kujinufaisha kwa kutegemea ukoo au nepotism. Rejea kashfa ya kuuzwa kwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambapo ushahidi ulionyesha kuwa waliokuwa makuwadi wa walioinunua walikuwa washirika wa shemejize rais. Hata huu wizi mkubwa katika sekta ya nishati na madini chanzo chake ni kwenye serikali hizi mbili. Pamoja na kwamba ufisadi ni kizalia cha mfumo wa kipebari usio na huruma, kuna ushahidi mkubwa kuwa mabaki ya ukoloni nayo yamechangia sana hasa nchi zinapokuwa zinaendeshwa na katiba zisizotokana na watawaliwa au hoi polloi.
        Tuje kwa Magufuli ambaye ameonyesha ujasiri na uzalendo wa hali ya juu unaoandamana na uchungu wa kuona Tanzania ikichezewa na kuliwa mbele na nyuma. Je atafanikiwa kwenye mapambano yake bila kuwa na katiba wezeshi na wananchi? Jibu analo Magufuli ingawa hataki kulikubali na kulitumia. Hapo tarehe 12 Juni, 2017, akipokea taarifa ya pili ya makinikia, alikaririwa akisema “ndugu zangu watanzania nimewambia nafanya hivi kwa ajili yenu…kazi [urais] ni ngumu sana… ndiyo maana tunaomba mtuombee…mimi muda wangu utapita.” Magufuli anakiri kuwa atapita na mfumo anaousimamia hauwezi kujiendesha. Kinachoshangaza ni namna anavyosuasua  au kuahirisha katiba mpya wa wananchi ambao licha ya kutumia fedha zao nyingi na muda, ilishafikia pazuri; na ilishapata maoni yao. Kwa wanaojua mchakato huu ulivyotekwa, kuvurugwa na kuchakachuliwa wanajua fika waliofanya hivyo hawakutaka iwatupe korokoroni tokana na ufisadi uliasisiwa na kusimamiwa na awamu zao. Sijui Magufuli anahofia nini wakati alishalionyesha taifa uzalendo wake? Pia, kama rais anajua kuwa atapita, sasa anashindwa au kuchelea nini kurejesha mchakato usiochakachuliwa wa katiba iliyopendekezwa na watanzania kwa maslahi yao na vizazi vijavyo; siyo kama kujipiga mtama? Wakoloni kwa kujua walichowatendea wengine, waliamua kuachana na katiba za kizamani na kutunga katiba ambazo zinaendesha nchi zao bila kutegemea utashi wa rais au awamu kama ilivyo Tanzania na nchi nyingi za kiafrika.
        Tumalizie kwa kumtaka Magufuli atumie ujasiri, usongo na uzalendo alioonyesha kwenye kupambana na ufisadi, kurejesha katiba ya wananchi ili isaidie si kupambana na ufisadi bali kuuondoa kutokana na kuwa na vifungu vinavyoshughulikia ufisadi na maadili ya viongozi kivitendo na kisheria. Bila katiba mpya ya wananchi, Magufuli atashindwa na anajipiga mtama kama wasemavyo watoto wa mjini.
Chanzo: Tanzania Daima Jumapili leo.

Wahamiaji Haramu: Kuna siku Tanzania itatawaliwa na mgeni

june 11
Baptista Marco raia wa Burundi aliyekamatwa nchini hivi karibuni akifanya kazi kama mwanasheria wa TBS kinyume cha sheria.

Matukio ya wageni kukamatwa wakifanya kazi nchini–tena nyingine nyeti–kinyume cha sheria yanazidi kuongezeka kiasi cha kuanza kujenga shaka juu ya usalama wa taifa na wananchi kwa ujumla. Hapa lazima tujiulize tatizo liko wapi; na nini kifanyike kuondoa hatari hii ambayo inaweza kutugharimu kama taifa. Wahenga walinena: usipoziba ufa, utajenga ukuta; jambo ambalo ni gharama baada ya nyumba kubomoka.

            Kuna matukio ambapo wakimbizi wa kiuchumi wa kigeni wamemeajiriwa nchini na kufanya kazi kwa muda mrefu bila kustukiwa. Je vyombo vyetu wa usalama vinafanya kazi gani na kama vinafanya kazi je vinaifanya vizuri? Mtu anaajiriwa kwa ngazi ya juu. Je anapataje kazi kama hakuna rushwa? Je wako wangapi wahalifu wa namna hii?

Je wako peke yao au wana mitandao ya watanzania wanaowasaidia kutekeleza jinai hii? Je mamlaka zinachukua hatua gani dhidi ya mitandao hii ambayo bila shaka itakuwa inajulikana?

            Japo mimi ni muumini wa umoja na ushirikiano vya kweli kwa Afrika, si mpenzi wa ushirikiano wenye kuvunja sheria ambapo baadhi ya wahalifu hujipenyeza kwenye nchi nyingine kinyume cha sheria na kujipatia kazi na elimu wakati wananchi wakikosa vitu hivi. Si mpenzi wa uchoyo wa baadhi ya mataifa hata watu kupenda kwenda kuchuma kwa wenzao bila kujali madhara wanayosababisha au bila kuruhusu watu kutoka huko wanakohujumu kwenda kupata kazi au kuishi kwenye nchi husika. Uumini wangu wa Afrika ni kwa nchi zote kuunganishwa na kurejea kuwa moja kama Afrika ilivyokuwa kabla ya kugawanwa na wakoloni kwenye mkutano wa Berlin 1884-85. 

Kwa taifa kuondokana na kadhia hii, kuna haja ya kutunga sheria kali zinazowapa adhabu ya vifungo virefu sana hawa wakimbizi wa kigeni waliojipenyeza na kupata kazi au elimu nchini kinyume cha sheria ili wasifaidi vitu hivyo nchini na nje ya nchi ama makwao. Pia wahalifu hawa wanapogundulika, wasipewe dhamana ili wasitoroke. Hapa ndipo umuhimu wa kubadili sheria ili kuondoa dhamana unajitokeza kama kweli taifa lina nia ya kuondokana na kadhia hii.  Maana uzoefu unaonyesha kuwa wengine hupewa dhamana na kutoroshwa na washitiri wao ili wasiumbuke kama ilivyotokea kwenye kashfa ya kutorosha wanyama hai kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro ikimhusisha mhalifu wa kipakistani ambaye alitoroshwa nchini.

Pia kuna haja ya mamlaka kujua; kwa sasa Tanzania inao raia wengi wa kigeni wanaoishi na kufanya kazi nchini kinyume cha sheria tokana na mfumo wetu mbovu na ile hali ya wananchi kutoelimishwa vya kutosha ili kusaidia kuwabaini wote wanaofanya hivi.  Haiwezekani watu wetu wakose ajira wageni wapate. Hapa lazima kutakuwa na tatizo kubwa mojawapo ikiwa ni ukosefu wa uzalendo na umakini katika kulinda mipaka na maslahi ya taifa letu. Nchi nyingine ukiingia tu, kila mtu anajua; na taarifa zako zinaifikia serikali mara moja. Tuachane na mambo ya kizamani. Kwani wakimbizi hawa wa kiuchumi wanadhoofisha uchumi wa taifa letu kiasi cha kufanya serikali ishindwe kutoa huduma bora kwa wananchi wake.

            Jingine, wote watakaobainika kutenda jinai wafilisiwe mali walizochuma nchini kwa kutumia elimu na fursa ya ajira nchini ili liwe somo kwa wengine wanaopanga kutenda jinai kama hii. Twende mbali; sambamba, tuwafunge waliowawezesha, kwa kuwahifadhi hata kuwatoza rushwa na kuwapatia ajira kinyume cha sheria.  Hapa lazima tuwe wakali na kuhakikisha kuwa yeyote anayeshirikiana nao , bila kujali cheo chake au uraia wake, anaadhibiwa vilivyo ili kuondoa uwezekano na vishawishi vinavyoshamirisha jinai hii nchini. Maana, tukiendelea na uhovyo na ulegelege huu, kuna siku Tanzania itatawaliwa na raia wa kigeni bila kujua; jambo ambalo ni hatari kwa usalama wa taifa letu.

           Kuondokana na kadhia hii, tuwabane marais wetu waunganishe nchi zetu ziwe nchi moja ili kuondoa kadhia kama hizi zinazoweza kuvuruga uhusiano wa mataifa.

            Tumalizie kwa kuitaka serikali hasa rais John Magufuli ambaye anasifika kwa juhudi zake za kuanzisha vita dhidi ya kughushi sifa na vyeti vya kitaaluma, apanue wigo hadi kuwashughulikia matapeli hawa wanaojipenyeza nchini na kupata elimu na kazi nchini bila stahiki yoyote kiutu na kisheria. Inatosha kusema kuwa wakati wa kuigeuza Tanzania shamba la baba inabidi ufikie mwisho. Hili litawezekana tu pale wananchi wetu watakapoelimishwa juu ya madhara yanayosababishwa na wakimbizi wa kiuchumi ambao wengi wao wanapata usaidizi toka kwa watanzania wenyewe wasijue wanajikomoa na kujichelewesha. Haiwezekani nchi yenye kila aina ya vyombo vya usalama iendelee kuhujumiwa kirahisi hivi huku vyombo husika vikipoteza muda kuwachunguza wapingaji, wapinzani na mambo mengine madogo badala ya kutoa kipaumbele kwa usalama wa taifa kwa maana ya usalama wa taifa badala ya kuwa usalama wa chama kama ilivyo kwa sasa ambapo vyombo vyetu vya usalama vinatumika vibaya.

Chanzo; Tanzania Daima Jumapili leo.