Tag: Kijiwe

Ufisadi: Kijiwe chataka haki sawa kwa wote

        Baada ya kutolewa onyo kali la hovyo kuwa tusiwaguse wakubwa mafisadi, kijiwe kimekaa kama kamati kulidurusu na kutoa angalizo kikizingatia sharti la katiba ya kaya kuwa kila mtu anastahiki haki na wachovu wote ni sawa. Hivyo, bila woga wala upendeleo, kijiwe kitatongoa na kudurusu baadhi ya masuala na kuyatolea majibu.
        Msomi Mkatatamaa anaingia akiwa na magazeti mengi tu. Anayaweka mezani na kuamkua na kusema “jamani mmesikia ujinga wa kutaka kutufundisha woga ili tuendelee kupigwa?” Anapiga hafa yakuendelea “katika maisha yangu sikutegemea kuwa wale wanaotuaminisha kuwa wanapigana na ufisadi kwa ajili yetu wangekuwa vigeugeu na woga kiasi cha kuogopa hata mawazo. Nani alitegemea kuwa majizi makubwa yaitwayo maheshimiwa yangekingiwa kifua wakati wanaofanya hivyo walituaminisha kuwa watatenda haki bila kujali itikadi, cheo, dini, kabila, eneo na makandokando mengine?”
        Kablaya kuendelea Mheshimiwa Bwege ambaye huwa hana tabia ya kuchomekea, anaamua kumchomekea na kusema “wewe uliamini rongorongo za wanasiasa wakati wakisaka kula ya kura siyo? Hujui kuwa baba na mama yao ni moja! Hata hivyo, kama tutakuwa wakweli, nani amkamate nani wakati wote ni watoto wa nyumba moja? Nani amshughulikie nani wakati wote ni sehemu ya tatizo ukiachia mbali hizi rongorongo za kutafutia umaarufu? Pamoja na ubwege wangu, sikushangaa hasa ikizingatiwa kuwa huku Afrika wateule huwa hawaguswi hata wanapopiga kama ilivyokuwa kwenye madili ya ANBEN, EPA, ESCROW, Richmonduli, IPTL na mengine, mnapaswa kula pini kwa vile jukumu lao ni kuwala na kuwatumia nyinyi.”
        Mgoshi Machungi naye anaamua kula mic “hata sisi hatishangai hasa ikizingatiwa kuwa hakuna kesi ya ngedee inaweza kushindwa mbee ya nyani. Mimi najua fika. Wengine sea zao ni za kuindana; na huu ndiyo wakati wa kufanya hivyo hasa ikizingatiwa kuwa tinaendeshwa kifaumefaume bia kujitetea tokana na woga na ujinga tena unaofanywa na wae unaoweza kudhani wamisoma wakati ni bue kabisa. Hamkuona madaktai wakijikombakomba kana kwamba hawakusoma?”
        Mpemba naye anakatua mic “yakhe hapa nkuunga nkono. Hata mie nilishangaa sana pale nilioposoma kuwa jarida fulani limefungiwa kwa kuchapisha picha za wateule wenye mazonge na kashfa. Wallahi mie ningependa wabadilishe katiba lau waseme kuwa ufisadi ni halali ya wanene na si wadogo kama hawa tuwaonao wakihangaishwa kwa vile walipiga tena kiduchu ikilinganishwa na hawa walotuuza hadi rahis akajikuta pakanga akishughulikia kashfa tu badala ya mambo mengine muhumi kwa kaya.”
        Mipawa anaamua kumpoka Mpemba mic “hapa lazima tukubaliane kuwa ufisadi si kosa  hasa linapotendwa na wakubwa, washirika, watoto hata wake zao kama ilivokuwa kwenye kashfa ya Kiwila na nyinginezo zinazokingiwa kifua wakati hata ndege wanazijua na kutushangaa kwa tunavyodanganyana kuwa twaweza kujenga kaya ya haki na ya maendeleo bila kutenda haki sawa kwa wote.”
        Kabla ya kuendelea, Kanji anampoka mic Mipawa na kudema “mimi hapana sangaa. Samaki vote iko na surubu. Hivyo, hapana samaki nasulubu menjake kwa kuwa na surubu. Kama nachunguza yote wizuri, nakuta iko na kashfa kama ile ya kuuja jumbani ya umma kwa vakuba chini ya hii moja nono nalinda sasa na naambia chowu kuwa iko wiwu va kufikiri. Halo halo natoka vachowu natoka Kapa!”
        Mijjinga aliyekuwa akibukua magazeti anaamua kutoa ya moyoni “mie naona tuache woga. Tuingie mitaani kudai tuambiwe kaya hii ni ya nani kati yetu na hao wateule wezi. Maana, wamekuwa wakitwambia kuwa kaya hii yetu na wao ni watumishi wetu. Huu ndiyo utumishi au wanatutumia wakimaanisha watumishi? Kwani hizo ofisi ni mali zao au za wachovu? Natamani marehemu Chris Mtikila angekuwa hai. Hapa pangechimbika bila jembe. Hata hivyo, sijui kama akina Tunda Jisu watakubali ghilba na vitisho hivi. Kwa ufupi ni kwamba tulianzishe kwa kuingia mitaani kudai uhuru wetu wa kutendewa haki na kusikika vingenevyo tutajikuta chini ya imla bila sababu zaidi ya woga na kujigongagonga kwa wale wanaobembeleza kitumbua uchwara kama yule daktari uchwara aliyefungia jarida kwa kuchapisha picha za wanene wenye mizogo ya kashfa.”
        Sofia Lion aka Kanungaembe anaamua kula mic “kwanza nilishangaa kusikia tishio na onyo kuwa waliopiga wakiwa kwenye ulaji wasiguswe wala kuandikwa kiasi cha kufungia jarida. Je wanasingiziwa; na kama wanasingiziwa kwani mahakama zimeisha kayani? Waende wakalalamike mahakamani badala ya kutumia mabavu bila sababu. Huu ni utumiaji mbaya wa mamlaka kusema ukweli. Hii ni kinyume na viapo vya uadilifu ambavyo mara nyingi wengi wamekuwa wakilishwa na wale wanaoweza kufanya mambo ya wachovu kuwa kama masuala yao binafsi wakichagua nani wa kuadhibu na nani wa kusamehe kama kwamba hii kaya ni falme la mja mmoja. Ni aibu hata ndege wanatucheka kwa kufanya kila jambo kuwa sanaa na sinema.”
        Kijiwe kikiwa kinachanganya si ukapita msafara wa Njaa Kaya akitoka zake kuzurura Ukanadani alikokwenda kuwapigia magoti wapiga wa makinikia bila kuwa makini. Acha tuuzomea na kutaka kupopoa kama si ndata kutuzidi nguvu.
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.