Tag: Kiswahili

Wizi wa Escrow tuanze na IPTK

            Hakuna utata; kampuni la the Independent Power Tanzania Limited (IPTL) ni donda ndugu kwa maendeleo ya uchumi wa taifa. Sitapenda kuongelea kesi iliyofunguliwa hivi karibuni dhidi ya watuhumiwa wa shilingi zipatazo bilioni 300 toka mfuko wa Escrow kwa vile iko mahakamani. Badala yake nitajadili namna ya kupambana na wizi huu ili taifa lisipate hasara tena.
            Kwa wanaojua namna kampuni tatanishi la IPTL lilivyoingizwa nchini kinyemela chini ya utawala wa awamu ya pili baada ya taifa kukumbwa na uhaba wa umeme kwenye miaka ya 90, watakubaliana nami kuwa ndilo chimbuko la wizi wa Escrow na hujuma nyingine ambazo zimekuwa zikiendelea dhidi ya taifa kwa zaidi ya miaka 20 hasa ikizingatiwa kuwa nusu ya wamiliki wake ndiyo wako mahakamani kwa tuhuma za wizi huu.
            IPTL ikiwa imeingizwa nchini na watawala wezi, ilianza kuhujumu taifa na Shirika la Umeme la Taifa (TANESCO) kiasi cha kuliua na kulifilisi hadi serikali ikawa inalikwamua huku wahujumu hawa wa uchumi wakiendelea kushika kani katika kuliibia na kulihujumu taifa. Pia, kutokana na hujuma hii, ambapo TANESCO iliuziwa umeme kwa bei mbaya, wateja wa nishati nchini walikuwa wakilanguliwa na kupandishiwa bei za umeme kila mara wakati taifa likiwa na vyanzo vingine imara kama vile maporomoko ya Stigler ambayo hivi karibuni rais John Magufuli alianza juhudi za maksudi kuyaendeleza ili taifa lijitosheleze kwa umeme na kuondoka kwenye mikono ya matapeli wa ndani nan je wanaotumia uhaba wa nishati kama mtaji na kijiko cha kutuhujumu na kutuibia. Baadhi ya vyanzo vyetu vinasema mradi huu ulizuiwa maksudi ili IPTL na makampuni mengine kama yale yaliyozaliwa na kashfa ya Richmond iliyozaa makampuni ya Dowan na Symbion kuendelea kuliibia na kulihujumu taifa. Nayo yanapaswa kushughulikiwa sambamba na IPTL. Kwani sifa na kazi zao ni moja tu, kuhujumu na kuliibia taifa.
            Kwanini tunasema kuwa bila kushughulika na IPTL mchezo utaendelea? Tuna sababu kuu zifuatazo:
Mosi, watuhumiwa wa kashfa ya Escrow walitumia IPTL hii hii pamoja na utata na kuisha muda wake kuliibia taifa. Inashangaza kwa kampuni ambalo limekuwa likihujumu taifa kuendelea kufanya biashara nchini ukiachia mbali kutochukuliwa kwa mali zake na uchafuzi wa mazingira ambao limekuwa likisababisha.
Pili, tunaambiwa IPTL inamilikiwa na watuhumiwa wawili kwa asilimia 50 ambapo asilimia zilizobaki zinamilikiwa na Simba Trust ambayo hata hivyo, tangu sakata hili lianze, huwa haitajwi hadharani. Je nani wamilki wa Simba Trust? Umma ungepaswa kuwajua ili nao waunganishwe kwenye kesi inayoendelea kwa vile isingewezekana wabia nusu wachukue mabilioni haya na wayatafune peke yake.
Tatu, kuna haja ya kutangazia watanzania kuwa IPTL haina uhalali tena wa kufanya biashara Tanzania hasa ikizingatiwa kuwa–licha utata wa mkataba wake na kushiriki uhujumu wa taifa–muda wake ulikwisha siku nyingi. Hapa lazima tuseme wazi kuwa IPTL ina washitiri na washirika nchini tena wenye madaraka. Rejea hivi karibuni Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) illivyotaka kuihalalisha IPTL kwa mara nyingine kwa kutaka watanzania wachangie maoni yao kabla ya kupewa leseni tofauti na makampuni mengine yanayofanya biashara nchini. Hivyo basi, serikali–licha ya kuwafichua Simba Trust–inapaswa kuwafichua maafisa wa umma na binafsi ambao wamekuwa wakiisaidia IPTL kuendelea kufanya biashara nchini kinyume cha sheria ukiachia mblai kuhujumu taifa. Haiingii akilini kuwa kampuni tapeli na la kigeni lingeweza kuendelea kuhujumu na kuibia taifa bila kuwa na watu wenye vifua serikalini na nchini kulikingia kifua. Mfano, wote walioshutumiwa kupokea mamilioni na mabilioni ya Escrow wanapaswa kukamatwa na kufikishwa mahakamani huku mali zao zikikamatwa ili kurejesha fedha ya umma. Na hapa tusisikie kelele za mawakala na makuwadi wao kuwa tunawatisha wawekezaji.  Hawa si wawekezaji bali wachukuaji wanaopaswa kunyolewa bila maji wala huruma kama walivyokuwa wakilifanyia taifa.
Nne, kukata mzizi wa fitina, sheria za nishati zibadilishwe ili kuzuia mianya ambayo ilitumiwa na makapuni kama IPTL kuliingiza taifa kwenye mdororo na mgogoro wa kiuchumi tokana na ulafi, ujinga na ufisadi wa watu wachache wasioona mbali.
Tuhitimishe kwa kupongeza na kuunga mkono juhudi mahsusi na za maksudi anazofanya na serikali ya rais Magufuli kuliondoa taifa kwenye mikono ya matapeli na wezi wanaorejesha maendeleo ya taifa na watu wake nyuma. Tunashauri wahusika wapewe adhabu kali ili liwe somo kwa wengine wanaodhani Tanzania ni shamba la bibi. Yote yafanyike; ila muhimu, bila kusambaratisha IPTL, ni kama tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu. Kwani kuendelea kuwapo kwake na makampuni yanayofanana nayo si tishio tu kwa uchumi wa taifa bali hata usalama wake.
Kwa miongo tuliyotapeliwa, kuibiwa na kuhujumiwa, kama taifa lenye watu wenye akili, tufikie mahali tukate mizizi ya fitina mojawapo ikiwa ni kampuni ya IPTL.
Chanzo: Tanzania Daima J’pili leo.

Kijiwe chataka kujua nini sharia za madini zitaanza kubadilishwa

            Baada ya rais Joni Kanywaji kusema atalazimisha Mjengo kukaa muda zaidi ili kurekebisha sharia za madini, Kijiwe kililipuka kwa furaha kabla ya kuzimika matumaini baada ya porofwedheha Joni kutoka Ukanadani kuja kuweka mambo sawa na kuuzima moto wa mabadiliko ya sharia.
            Msomi Mkatatamaa siku hizi anaingia mapema akiwa na inshu kibao. Akiwa amesheheni mzigo wa magazeti anayokopa kwa muuza magazeti anautua mezani na kuamkua na kusema “wenzangu mnasemaje kuhusiana na ahadi ya kuuamrisha mjengo ubadili sharia za madini na mafuta ili kupambana na upigaji ulioigeuza kaya yetu makinikia? Naona kama sakata la Escrew limefuta kila kitu kana kwamba lina thamani kuliko madini na nishati ingawa nalo ni sehemu ya nishati. Sijui wenzangu mna mikakati gani ya kuwarejesha hawa ambao wanaonyesha kuwa wepesi wa kusahau na kulaghaiwa kwa ahadi za maongezi hadi kutelekeza ubadilishaji wa sharia?”
            Mijjinga anakula mic ‘mie naona mambo mengi yanaendeshwa kizimamoto tena kwa kutegemea usongo wa dingi lakini si kaya. Namna hii tutaendelea kupigwa; kwa sababu tunaonyesha kama hatuko serious wala hatuna maandalizi. Kama unakumbuka waraka uliotolewa juzi na jambazi akashia kuwa hawakukubaliana kurejesha njuluku zetu, basi unaweza kuelewa anachohofia Dk Msomi. Hivyo, napendekeza tuandike waraka maalumu kwa dingi kukumbushia ubadilishaji wa sharia na kuwanyonga wale waliotuingiza kwenye mkenge hadi tukapigwa kijinga hivi.”
            Mpemba anampoka mic na kudema “yakhe nami nkuunga nkono. Kama tutaendelea kukubali kila jambo wallahi tutajaendeleapigwa bila sababu bali ulimbukeni wa baadhi ya wale waniofanya vitu kwa kukurupuka. Hata hivo, kama dingi atakumbushwa, naamini atarejea nchakato huu wa ukombozi wa kaya yetu.”
            Kabla ya kuendelea Mipawa anampoka mic na kusema “hakuna cha kurejea nchakato. Uko wapi ule wa Katiba Mpya ambayo ilikuwa muarobaini wa kila kitu. Si imeuawa ili kuendelea kulindana na kukomoana kwa kufanya mambo kwa akili ya chama kimoja wakati wa utawala wa vyama vingi. Kusema ukweli mie sina imani na chochote wala lolote hadi nione sharia zikibadilika na kurejewa kwa mchakato wa Katiba Mpaya.”
            Kapende aliyekuwa akibofya ki-Samsung chake anaamua kutia guu na kusema “mie simlaumu dingi hasa ikizingatiwa kuwa ameachiwa afanye kila kitu kana kwamba hana wasaidizi. Ninachoona akisaidiwa si chochote wala lolote bali kumuimbia kwaya ya sifa kiasi cha kukera na kuchusha. Hakuna ninapoumia kama kuona madaktari na hata maprofwedheha wakimsifia hata pale anapotimiza wajibu wake. Hapa kweli ipo shughuli. Nadhani sisi tujichukulie wadhifa wa kumshauri dingi baada yakuona aliodhani wangefanya hivyo kumgwaya kila mmoja akitetea kitumbua chake hata kama ikibidi kwa kujikomba.”
            Kanji naye anaamua kukamua, “veve sangaa vatu jipendekeza. Kama hapana pendekeza kupendeza dingi nataka afukuze yeye veve tampa juluku na laji nakula bure? Kama profesa napendekeza veve nani hapana pendekeza. Basi naji jiwe pendekeze ilete katiba mpya ya vananchi ili mambo yote ive safi au vipi dugu yanguni?”
            Sofia Lion aka Kanungaembe anatia timu na kuchonga “kwa vile sisi si wateule wala wajipendekezaji na waimba sifa, lazima tuseme ukweli. Kwani hatuna cha kupoteza. Ninachomaanisha hapa ni kwamba kama hawatabadili sharia za mimawe na mifuta kila kitu ni bure. Ni sawa na kutwanga mawe. Nadhani hawa jamaa waliwahi kuja kujifanya wanajutia kosa lao na wako tayari kutapika njuluku ili kutuzuga tupoteze muda wakati wakijiandaa kutushikisha adabu.”
            Mheshimiwa Bwege anamchomekea da Sofi na kukwangua mic na kudema “Sofia umejuaje kuwa ilikuwa nawaza kusema uliyosema. Nakubaliana nawe mia kwa mia kuwa hawa jamaa wanataka kuendelea kutugeuza mabwege. Wanafanya kile ambacho watasha huita to buy time as you contemplate how to thwart your enemy outfront.”
            Kabla ya kuendelea mzee Maneno anamkatiza kwa kusema “Mheshimiwa Bwege lugha hiyo naona kama imepiliza.”
            Kila mwanakijiwe amepigwa na butwaa ile mbaya hasa ikichukuliwa kuwa hii ni mara ya kwanza kwa mheshimiwa Bwege kumwaga ung’eng’e. Wengi tulidhani haupati kumbe kifaa! Tena anaongea ung’eng’e mufti bila kubukanya na kuchanganya na broken.
            Mheshimiwa Bwege anaendelea kuchonga “samahanini kwa kuongea kingindo ndugu zanguni. Ibidipo hubidika. Nilidhani nilikuwa kwa mama wa ukoloni kule Londoni kumbe niko hapa Danganyika nikidanganyika kama kawa. Tusameheane sana ndugu zanguni. Yote yalinitoka katika ile hali ya kutoa mchango kwa kaya yangu ili kuiepusha na kupigwa pigwa na kugeuzwa shamba la bibi.”
            Mgosi Machungi ambaye aliingia akiwa amechelewa na akawa anafuatilia mjadala kwa makini anaamua kutia guu “wagoshi tikubaiane kuwa bia kuandamana kushinikiza kuejea mchakato wa kubadii shaia tinapoteza muda. Nadhani tokana na ukapa, baada ya jamaa kutiahidi wangeipa njuuku yetu, timeangaia kupata si kupatikana. Titakapopatikana ndipo titajua. Na hapo utasikia wanasiasa wakitafuta kia kisingizio ili tione hawana makosa.”
            Kijiwe kikiwa kinanoga si likapita shangingi la dingi wa Akashia. Acha tumtoa mkuku ili tumfanyie kitu mbaya kabla ya kwenda kutaifisha migodi yetu!
Chanzo: Tanzania Daima Jumatano leo.

Natamani Tanzania ingekuwa Korea ya Kusini

       Hivi karibuni, nchi ya Korea ya Kusini iliingia kwenye historia ya dunia kwa kuwa miongoni mwa nchi zinazopambana na ufisadi mkubwa bila huruma kuonea. Rais wa zamani wa nchi hiyo Park Guen-hye alijikuta akiondolewa madarakani na kusindikizwa gerezani anakongojea kusikilizwa shauri lake la kuruhusu rafiki yake Choi Soon-sil kutumia ofisi ya rais kujitajirisha kinyume cha sheria. Choi ambaye naye yumo gerezani akingojea kusikilizwa kesi yake, alitumia ukaribu wake na rais kuyasumbua makampuni mengi ya kibiashara kuchangia asasi yake isiyo ya kiserikali ambapo kipindi kimoja, alilazimisha kampuni ya Samsung kuchangia dola za kimarekani 69. Wakati akiingizwa gerezani hapo tarehe 31 Machi, 2017 bango moja lilimpokea likisema “hongera kwa kuingia gerezani. Toka ukiwa binadamu baada ya miaka 30.”
        Park angekuwa rais wa kiafrika, nani angemgusa.  Asingeondoshwa madarakani kwa aibu na kuishia korokoroni. Angetafutiwa mazingira ya kumlinda hata baada ya kuthibitika kuwa alitenda ufisadi. Lakini kwa wenzetu hilo hakuna. Hakuna aliyeko juu ya sheria; wala anayeruhusiwa kutumia ofisi yake kwa manufaa binafsi kama ilivyo kwa Afrika ambako marafiki, watoto, wake au waume na ndugu wa viongozi nao hujipachika uongozi kwa sababu wazazi au ndugu zao ni marais.
        Hakuna ubishi. Kwa sasa, Tanzania inakumbwa na kashfa kubwa tu zinaohusisha hasara za mabilioni zilizosababishwa na baadhi ya watawala wetu na wasaidizi wao ima tokana na uroho, ujinga na ufisadi au roho mbaya kama siyo ulimbukeni. Kashfa hizi si mpya. Kinanchofanyika ni baada ya rais wa awamu ya tano John Pombe Magufuli kuingia madarakani na kufanya ambacho karibia watangulizi wake wote walishindwa kufanya–kuanza kufukua kila aina ya uoza–na kuchukua hatua hata kama si kwa wahusika wote. Zoezi la Magufuli la kupambana na ufisadi nchini limevutia wengi ingawa pia linakosolewa na wengi kutokana na kuhangaika na vidagaa huku mapapa wakisazwa. Wanaomuunga mkono Magufuli wanaona kuwa amethubutu. Wanaopinga harakati zake japo si wengi, wanaona kama hafanyi mambo kisayansi na hayawezi kuwa endelevu hasa kutokana na mfumo wa kikatiba wa kutekeleza haya ukiachia mbali mapungufu kama upendeleo wa baadhi ya watu wa karibu wake kama ilivyotokea kwa mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam Paul Makonda anayetuhumiwa kughushi vyeti vya kitaaluma.
        Mbali na Makonda, juzi baadhi ya wabunge wa upinzani waliposhinikiza kuwa marais wastaafu walioshiriki uoza na uovu huu washughulikiwe. Vyombo vya habari vilimkariri mbunge Kilombero (Chadema) Peter Lijualikali akisema “Haiwezekani mzee wangu (Andrew) Chenge na (Nazir) Karamagi walipitisha mikataba hiyo bila Rais aliyekuwapo kufahamu. Kinga ya Rais kushtakiwa iondolewe ili wahojiwe.” Baada ya Lijualikali kutoa pendekezo la kuondoa kinga kwa marais, spika wa Bunge Job Ndugai alisikika akiwaonya kwa kusema “Mabadiliko mnayoyataka yakipitishwa na viongozi mlionao wakikamatwa msije mkalalamika tena” akimaanisha mawaziri wakuu wastaafu Edward Lowassa na Fredrick Sumaye waliohamia kwenye kambi ya upinzani. Hapa unaweza kuona namna kulindana kulivyo tatizo la kimfumo zaidi. Badala ya spika kutumia mamlaka yake kuunga mkono haki ya kutenda haki, anaonekana kutoa vitisho kama ishara ya kuonyesha kuwa wapo wasioguswa. Hata hivyo, spika alisahau kitu kimoja kuwa hao mawaziri anaotishia nao watasombwa hawana kinga kama marais wastaafu ambao kimsingi ndicho chanzo cha ufisadi, uovu na uoza huu uliofanya taifa lenye kujaliwa raslimali lukuki kuwa maskini na ombaomba bila sababu zaidi ya ubinafsi, uchoyo, uroho na roho mbaya za baadhi ya watawala wetu waliogeuza ikulu kuwa chimbo la utajiri badala ya kuwa hekalu la haki la wananchi. Ingekuwa Korea ya Kusini, kauli ya spika ingemgharimu. Kwani, ameonyesha wazi kuunga mkono ufisadi.
        Naye mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu wala hakuficha wala kuzungusha. Alitaka rais Jakaya Kikwete ashitakiwe kwa vile ndiye aliingia mkataba wa mgodi wa Bulyankhulu tarehe 5 Agosti, 1994. Na wakati ule hakuwa na kinga yoyote kisheria. Je rais atawashughulikia watagulizi wake na nani yuko tayari kumvisha paka kengele zaidi ya yeye aliyeanzisha na anayesimamia mchakato huu? Maana, ukiangalia ushahidi uliopo, mambo mengine hayahitaji hata uwe mtaalamu wa sheria wala msomi kujua kuwa kinachoenda kufanyika ni kinyume na common sense. Sijui tunatoa taswira gani kwa wananchi wetu na vizazi vijavyo kwa kupendeleana na kulindana hata katika maovu?
        Kwa taifa linalotaka kujikomboa tokana na ufisadi lazima tujenge utamaduni wa kuhoji kila mtu bila kujali cheo chake. Wengi walidhani kama wahusika wanasingiziwa, wangejitetea na kuwataka wanaowatuhumu watoe ushahidi; wakishindwa wawajibishwe. Haiwezekani  rais awe mlalamikaji, mwendesha mashitaka, shahidi, haki na polisi. Kufanya hivyo, licha ya kuwa kinyume cha sheria, kunakinzana na ahadi za rais za kuwatendea watanzania haki bila kujali ukubwa wa cheo cha mtu.
        Tumalizie kwa kusema kuwa Tanzania inakabiliwa na matatizo yasiyo ya kawaida yanayohitaji majibu yasiyo ya kawaida yatokanayo na busara, ukweli, uwazi na ithibati vya aina yake. Siku zote huwa tunasikia watu wakiambiana wafanye maamuzi magumu. Korea Kusini walichukua maamuzi magumu. Nasi kama taifa, kama kweli hatuwadanganyi watu wetu na kuwageuza hamnazo, tunapaswa kufanya maamuzi magumu kwenye kupambana na ufisadi bila upendeleo wala kutishana. Natamani Tanzania ingekuwa Korea Kusini.
Chanzo; Tanzania Daima Jumatano leo